HOT NEWS

    Featured Posts

Loading...

KUTOKA MOSHI:..CHADEMA JANA IMEUWASHA MOTO HUKO MOSHI KWA WANAOSALITI CHAMA HICHO


Moshi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza kuwasakama madiwani wanaodaiwa kukisaliti katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Katika uchaguzi wa meya uliofanyika Desemba 16, mwaka jana madiwani wawili wa chama hicho walidaiwa kukisaliti na kumpigia kura mgombea wa CCM, Priscus Tarimo. Hata hivyo, katika uchaguzi huo uliokuwa na wajumbe 30, mgombea wa Chadema, Raymond Mboya aliibuka kidedea kwa kupata kura 22, huku Tarimo akipata tano.
Tafsiri ya matokeo hayo ni kuwa kama madiwani wa CCM katika baraza hilo wako watatu na mgombea wao alipata kura tano, ni wazi madiwani wa Chadema walimpigia.
Wiki iliyopita Kaimu Katibu wa chama hicho katika manispaa hiyo, John Minja aliwaandikia barua madiwani wanaodaiwa kufikia watano wakituhumiwa kuhusika na usaliti huo na kutaka wajieleze.
“Baada ya kusoma taarifa ya kamati ya uchunguzi imeonekana wewe ni mmoja kati ya madiwani waliokisaliti chama wakati wa uchaguzi wa meya na naibu meya,” ilisomeka sehemu ya barua waliyopelekewa.
Barua hiyo ilitumwa kwa madiwani hao kila mmoja na nakala yake, ikidai kitendo hicho kilikiuka katiba ya chama na kanuni za madiwani wa Chadema ibara ya 5.0 vifungu vidogo vya (a) na (c).
“Kamati ya utendaji kwa mamlaka iliyonayo inaagizwa kuleta utetezi wako ndani ya siku 14 kuanzia tarehe unapopokea barua hii. Mwisho wa kupokea utetezi ni tarehe 04.02.2016,” ilisema barua hiyo. Hata hivyo, baadhi ya madiwani wanadai kuwapo kwa mpango mahususi wa kuwaondoa wasiomnyenyekea mmoja wa viongozi, jambo ambalo hawatakubali.
“Kwanza kura zilipigwa kwa siri, hivi unajuaje nani alimpigia nani? Hiki kinachofanyika ni kututisha lakini hatutabadilika na tunazijua vizuri haki zetu,”alidai mmoja wa madiwani hao.
Madiwani hao ambao waliomba majina yao yasitajwe walidai hata uamuzi wa kumsimamisha Katibu wa Chadema wa manispaa hiyo, Steven Buberwa ni mwendelezo wa kukigawa chama.
Mwenyekiti wa Chadema Manispaa ya Moshi ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffar Michael alisema bado hawajafikia hatua za kuwachukulia hatua madiwani na kinachoendelea ni uchunguzi.

HABARI NZITO:...WATU WANAODAIWA NI MAJANGILI WATUNGUA HELKOPTA NA KUUA RUBANI

Watu wanaodaiwa kuwa ni majangili na wawindaji haramu wameitungua kwa risasi helkopta ya doria ya wanyamapori katika pori la akiba la maswa lililoko wilaya ya Meatu mkoani Simiyu kusini mwa hifadhi ya taifa ya Serengeti na kumuua rubani wa helkopita na kumjeruhi askari mmoja wa wanayamapori.
Kufuatia tukio hilo, waziri wa maliasili na utalii Profesa Jumanne Maghembe amefika katika eneo la tukio na kusisitiza kwamba serikali kwa kushirikiana na vyombo vyote vya dola na vyombo vya ulinzi na usalama inaanzisha mkakati mpya wa kupambana na ujangili na uwindaji haramu wa maliasili ikiwemo Tembo ambao ni rasilimali muhimu kwa taifa na kwa uhifadhi wa taifa la Tanzania.
Waziri Maghembe ambae amefika kwenye eneo hilo ilipotunguliwa helkopita hiyo katika safari iliyokuwa na msukosuko mingi ya barabara na hasa kipindi hiki cha mvua na kuikuta helkopita iliyokuwa inarushwa na kepten Roger Gower raia wa Uingereza ambae alifariki baada ya kujeruhiwa kwa risasi amesema tukio hilo limewakera wadau wote wa uhifadhi na serikali kwa ujumla na kamwe haliwezi kuachwa lipite bila hatua madhubuti kuchukuliwa huku akiwaonya baadhi ya watumishi wa serikali na askari wa wanyamapori wanaoshirikiana na wahalifu kuwa sasa kiama chao kimefika.
Nae kamanda wa upelelezi wa mkoa wa Simiyu Jonathan Shana amesema tukio hilo lilitokea jana jioni wakati helkopita hiyo ikiwa katika doria baada ya kusikika milio ya risasi ya majangili katika pori hilo ambapo Tembo watatu waliuwawa na kwamba watu watatu wanashikiliwa na polisi wakihojiwa kufuatia tukio hilo ambapo mkurugenzi mkuu shirika la hifadhi za taifa Tanzania Tanapa Allan Kijazi amesisistiza umuhimu wa wadau kuongeza nguvu katika kukabiliana na matatizo ya ujangili nchini.

MBUNGE WA CHADEMA ACHANIWA SUTI YAKE NA POLISI

 Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Peter Lijuakali akitolewa bungeni na polisi.
Na Mwandishi Wetu, Risasi Jumamosi..

DODOMA: KALI ya mwaka. Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Peter Lijuakali wa Chadema, amechaniwa suti mbili katika matukio mawili tofauti na Jeshi la Polisi ndani ya wiki moja, Risasi Jumamosi linakutaarifu.

Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Peter Lijuakali..

Katika tukio la kwanza, mbunge huyo alitolewa nje kwa nguvu kutoka Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, baada ya kukaidi agizo la mwenyekiti wa kikao, Yahaya Nania la kumtaka asishiriki katika zoezi la kuapishwa kwa madiwani wateule na kumchagua mwenyekiti na makamu wa halmashauri hiyo kwa kili kilichodaiwa kuwa hakuwa mjumbe halali wa baraza hilo.

Katika purukushani hizo, zilizotokea Januari 24 mwaka huu, ambazo yeye aligoma kutoka akidai ni mwakilishi halali wa wananchi wa jimbo lake, mbunge huyo alichaniwa suti yake katika vuta nikuvute ya polisi.

Katika tukio la pili, Januari 27, mwaka huu, lililosababisha suti yake nyingine kuchanwa na polisi, Lijualikali alikuwa mmoja wa wabunge wa upinzani waliotolewa nje kwa nguvu, baada ya kukaidi amri wa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge ya kukaa chini na kutulia.

Wabunge hao walichukuliwa hatua hiyo baada ya kupinga kujadiliwa kwa hotuba ya rais, aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa Bunge Novemba mwaka jana, wakitaka kwanza kupata ufafanuzi wa serikali kwa kitendo chake cha kulizuia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kurusha vipindi vyote vya vikao vya Bunge moja kwa moja (live).

Kana kwamba haitoshi, wabunge wa upinzani kwa mara nyingine walitoka nje ya Bunge katika kikao chake cha asubuhi, Alhamisi iliyopita baada ya Naibu Spika, Tulia Akson kukataa kusikiliza mwongozo uliokuwa ukiombwa na wapinzani, baada ya Naibu huyo kuzuia kujibiwa kwa swali la mmoja wao kuhusu elimu ya bure.

HABARI YA HIVI PUNDE:..(VIDEO)..RAIS MAGUFULI AFANYA KUFURU YA MWAKA KWA MKUU WA MAJESHI NCHINI "JENERALI MWAMUNYANGE" NA HII HAIJAWAHI KUTOKEA TZ, MKUU WA MAJESHI APIGWA MIAKA KADHAA NA RAIS

Rais John Pombe Magufuli amemwongeza muda wa mwaka mmoja zaidi Mkuu wa Majeshi Nchini Jenerali Davis Mwamunyange kuendelea kuongoza Jeshi. Full stori ipo kwenye hii video hapa chini



ZITTO KABWE: SERIKALI YA AWAMU YA 5 IMEANZA NA MGUU MBAYA,ISIPOJIPANGA UPYA ITAENDELEA KUAIBIKA

 

Kauli za Zitto Kabwe Asubuhi ya leo Facebook;

"Serikali ijue kuna Bunge. Bunge lina wabunge makini na wenye mapenzi ya dhati kwa Taifa letu. Serikali isipojipanga upya itaendelea kuaibika" 



"Bunge limeiamuru Serikali kuleta Mpango wa Maendeleo. Shughuli ya kwanza ya Serikali Bungeni imeondolewa kwa hoja kutoka Upinzani. Serikali ya Awamu ya 5 imeanza na mguu mbaya. Wajue Bunge lipo. Hatuburuzwi"

BREAKING NEWS:..SHAMBA LA WAZIRI MKUU STAAFU SUMAYE LILILOVAMIWA NA WANANCHI LAIBUA MAZITO TENA, SERIKALI YATOA TAMKO ZITO


WAZIRI Mkuu Mstaafu Mhe. Fredrick Sumaye, ameiangukia serikali na kuomba msaada baada ya wananchi kuchukua sheria mkononi na kuvamia eneo lake la ekari 33 lililopo Mabwepande katika Manispaa ya Kinondoni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.



Serikali imemuahikikishia Mhe. Sumaye kuwa haina mpango wa kumkandamiza mtu mnyonge wala tajiri hivyo itahakikiha inatoa haki kwa kila mmoja baada ya wiki mbili kwa kua imesikiliza pande zote mbili katika mgogoro huo. 

Akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya wananchi wa kitongoji cha Kimondo mtaa wa mji mpya Kata ya Mabwepande na Mhe. Sumaye Dar es Salaam jana asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda alisema ili kumaliza mgogoro huo ambao Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye ameiomba serikali kuingilia kati ni lazima busara kutumika. 

Alizitaka pande hizo mbili kuiachia serikali kwa wiki mbili ili kutafuta njia bora ya kumaliza tatizo hilo huku wananchi wakitakiwa kuacha kuendelea na ujenzi na kugawiana maeneo katika shamba hilo. 

“Serikali ya Rais Magufuli ni sikivu na ndio maana ilikuwa tayari kumsikiliza Waziri Mkuu wetu Mstaafu Sumaye na kusikiliza wananchi. ili kutenda haki tunatambua migogoro ya ardhi ilivyokuwa na athari kwa jamii hatuna mpango wa kumkandamiza tajiri wala mnyonge,”alisema. 

Alisema katika eneo hilo anajua jinsi wananchi walivyotumia nguvu katika kuwekeza ujenzi na rasilimali zao lakini kwa sasa wasitishe shughuli hizo na kuendelea kugawana maeneo na Sumaye pia kuacha uwekezaji ili kutafuta suluhu. 

"Zipo njia nyingi tutazitumia kumaliza mgogoro huu ikiwemo kufuata sheria kwa kuangalia iwapo mzee wetu alikiuka taratibu za kumiliki ardhi kama ilivyodaiwa na wananchi ili tujue hatua za kuchukua,”alisema. 

Alisema pia wanaweza kukaa na Sumaye na kuzungumza naye ili kukubali hasara kwa kutoa eneo kidogo na kuwapatia wananchi hao ambao hawana makazi au Manispaa kutafuta eneo mbadala na kuwauzia kwa bei nafuu. 

Alizitaka pande hizo mbili kutambua umuhimu wa kulinda amani katika mgogoro huo kwa changamoto zilizopo kutatuliwa bila kutumia nguvu. 

Makonda pia aliagiza serikali ya kijiji kufanya utambuzi wa wananchi hao wenye makazi katika shamba la Sumaye. 

Awali katika mkutano huo Mhe. Sumaye alimueleza Mhe. Makonda jinsi serikali ilivyo na kazi ngumu ya kushughulikia migogoro ya ardhi na kuomba kutumia busara zake kumpatia eneo hilo analomiliki kihalali. 

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kama nilivyokueleza awali serikali yetu inakazi ngumu sana hasa kutokana na viongozi wa chini kutokuwa wasikivu na wakweli .Eneo hili namiliki kihalali ,nina nyaraka zote na ninalipia kila mwaka na nilikuwa katika mpango wa kutafuta wafadhili ili kuliendeleza kwa kujenga Chuo Kikuu,”alisema. 

Alisema yeye na familia yake waliuziwa eneo hilo toka mwaka 1997 na anaamini serikali itatenda haki. 

Diwani wa kata hiyo Suzan Masawe alisema anauthibitisho kuwa eneo hilo lilikuwa pori na Sumaye alilitelekeza kwa muda mrefu na kusababisha uhalifu ikiwemo wanawake kubakwa,mali za wizi kufichwa na uhalifu mbalimbali. 

Alisema kutokana na hatua hiyo walimtafuta Sumaye lakini hakuwa na ushirikiano kwakuwa hata alipofanya uwekezaji kwa kuchimba kisima cha maji alikataa kuwapa wananchi . 

Suzan alisema kutokana na hasira za wananchi hao kwa kukosa huduma za kijamii kwa muda mrefu ikiwemo eneo hilo kutokuwa na shule,Zahanati wala kituo cha polisi waliamua kuvamia na kujigawia maeneo. 

Mmoja wa wananchi hao Athuman Mnubi alikiri kweli hawana umiliki halali wa eneo hilo na katika hatua ya kutafuta makazi walivamia msitu huo uliotelekezwa na Sumaye. 

Alisema wanaamini kutokana na ahadi ya serikali ya Rais Magufuli katika kupora maeneo yaliyotelekezwa na wawekezaji watasaidiwa. 

WAKATI huo huo Makonda alisimamisha na kukamata baadhi ya malori ya kokoto na mchanga, wafanyakazi na Mwekezaji wa kigeni kutoka India Sules Waljan wanaochimba mchanga,kokoto na kifusi katika eneo la Mabwepande. 

Hatua hiyo imekuja baada ya kuona uharibifu mkubwa wa mazingira na alipowahoji wafanyakazi na Mwekezaji huyo kama wanavibali walisema hawana. 

Makonda amewafikisha watuhumiwa hao kituo cha polisi cha Wazo Hill ili kutoa maelezo ya kina na kusema kuwa serikali inatumia gharama kubwa kwa uhalibifu huo wa mazingira ambao pia unafanywa katika vyanzo vya maji na matengenezo ya madaraja yanayoharibiwa ni makubwa.

RAIS MAGUFULI AWAAPISHA BALOZI NA MAKATIBU TAWALA WAPYA NA MNADHIMU MKUU WA JWTZ

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 30 Januari, 2016 amewaapisha Balozi, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania na Makatibu Tawala wawili, Ikulu Jijini Dar es salaam. 



Walioapishwa ni: 
Balozi Mahadhi Juma Maalim, ambaye anakuwa Balozi mpya wa Tanzania nchini Kuwait. 


Luteni Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, ambaye anakuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Jenerali Samuel Albert Ndomba, ambaye amestaafu. Kabla ya Uteuzi huu Luteni Jenerali Mabeyo alikuwa Mkuu wa Usalama na Utambuzi wa Jeshi la wananchi Tanzania. 


Kamishna Paul Moses Chagonja, ambaye anakuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, akijaza nafasi iliyoachwa wazi Madeni Kipande ambaye uteuzi wake ulitenguliwa. 


Kamishna Clodwig Mathew Mtweve, ambaye anakuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Faisal Issa ambaye uteuzi wake ulitenguliwa. 


Akizungumza baada ya kuapishwa, Balozi Mpya wa Tanzania nchini Kuwait Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim, ameahidi kuiwakilisha vyema Tanzania nchini Kuwait hususani katika uchumi ili Tanzania iweze kunufaika na ushirikiano uliopo baina ya mataifa haya mawili. 


Nae Mnadhimu Mkuu wa Jeshi wa wananchi Tanzania Luteni Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, ameahidi kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na Mtangulizi wake Luteni Jenerali Mstaafu Samuel Albert Ndomba ya kuhakikisha anamshauri vizuri Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na hivyo kuliwezesha Jeshi hilo kutekeleza wajibu wake ipasavyo. 


Kwa upande wao, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Kamishna Clodwig Mathew Mtweve na Katibu wa Mkoa wa Katavi Kamishna Paul Moses Chagonja, wameahidi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa katika kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye mikoa waliyopangiwa, ikiwemo kusimamia nidhamu kwa watumishi wa umma. 


Gerson Msigwa, 
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU 
Dar es salaam 
30 Januari, 2016

BUNGENI HAKUKALIKI TENA MUDA HUU!:UKAWA MWENDO NI ULE ULE ,WATOKA NJE YA BUNGE...ASKARI WA KUTULIZA GHASIA WATANDA UKUMBI WA BUNGE TENA.

bwege akizomea
WABUNGE wa kambi ya upinzani jana walitoka bungeni, huku ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa katika viunga vya Bunge, MTANZANIA linaripoti.
Hatua hiyo ilitokea baada ya kipindi cha maswali na majibu pamoja na maswali kwa Waziri Mkuu alichokiongoza Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

Wabunge hao wa kambi ya upinzani inayoundwa na wabunge wengi kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walitoka nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kutaka mwongozo wa mambo mbalimbali jambo lililokataliwa na Naibu Spika Dk. Tulia.
Hatua hiyo ilikuja mara baada ya Dk. Tulia kutoa taarifa kuhusu ajali ya kivuko cha Mto Kilombero kilichozama juzi, ambapo Serikali ilitoa kauli juu ya tukio hilo.
Wakati Naibu Spika akitoa maelezo hayo, baadhi ya wabunge wa upinzani walisimama na kuomba mwongozo.
Hata hivyo Dk. Tulia alimpa nafasi Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kuomba mwongozo wake.
Matiko alitumia kanuni ya 68(7) na 63(1) akidai Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema uongo bungeni alipokuwa akifafanua kuhusu utoaji wa elimu bure.
“Kwanini Waziri Mkuu anatoa maelezo ambayo hana uhakika nayo? Kwa mfano kule jimboni kwangu kule Tarime, wanafunzi wa bweni wanatakiwa wapeleke chakula magunia ya mahindi na mwisho wa siku michango inafikia Sh 500,000, iko wapi dhana ya elimu bure?” alihoji Matiko.
Akijibu mwongozo huo, Dk. Tulia alisema tayari ufafanuzi ulishatolewa ya kuwapo kwa changamoto ya utoaji wa elimu bure.
Hata hivyo, kauli hiyo iliibua mzozo zaidi baada ya wabunge wa upinzani kuinuka na kudai miongozo zaidi.
Mbali na Matiko wengine walioomba mwongozo huo ni Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara wote wa Chadema.

Wabunge hao waliendelea kusimama na kupiga kelele wakiomba mwongozo na baadae kiti kilipoelekeza shughuli nyingine, wabunge wote wa upinzani walisimama na kuondoka wakiongozwa na Kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).

ULINZI MKALI BUNGENI
MTANZANIA lilishuhudia askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) zaidi ya 15 wakirandaranda katika viwanja vya Bunge, na wengine wakiwa wamesimama na kutanda katika milango yote ya kuingia bungeni.
Kuimarishwa kwa ulinzi huo kumetokana na hali ya juzi, ambapo Bunge lilichafuka wakati wa jioni pale polisi walipoamriwa kuingia ukumbini kuwatoa wabunge wa upinzani waliokuwa wakipinga kauli ya Serikali ya kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).

BULAYA
Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, alishangazwa na uwepo wa wingi wa polisi bungeni na kusema ni aibu katika karne ya sasa Bunge kuendeshwa kwa mtutu wa bunduki.
“Tumetoka kuonyesha hatukubaliani na uamuzi wa Serikali wa kuzuia matangazao ya Bunge yasiende ‘live’ (moja kwa moja). Wamejipanga kwa wingi wao kukandamiza haki ya wananchi ya kupata habari.
“Sisi tunajua, huu ni mkakati mpana utakaovikumba hadi vyombo vingine, TBC ni mwanzo tu, lakini hili ni tatizo, hapa si tu wananyima haki za wananchi, lakini wanakandamiza uhuru wa vyombo vya habari,” alisema.

LIJUALIKALI
Kwa upande wake, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali, alisikitishwa na hatua ya Naibu Spika kumnyima nafasi wakati akiomba mwongozo wa kiti.
“Mara baada ya Waziri Mhagama kutoa taarifa ya ajali ya kuzama kwa Kivuko cha Kilombero, nilisimama kuomba mwongozo ili nitoe taarifa nilizokuwa nazo kuhusiana na tatizo hilo.
“Nilipokuwa nikiomba nafasi nilidhani hawanijui, nikasema mimi ndiye Mbunge wa Kilombero kwa ‘attention’ zaidi, lakini bado sikusikilizwa.
“Nilitaka kutoa taarifa kwamba waziri amedanganya, yeye anasema watu 30 wameokolewa, lakini taarifa nilizonazo mimi nimepigiwa simu na wananchi jimboni kwamba kuna watu wamefariki dunia,” alisema.

KUBENEA
Naye Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, alisema: “Kutoka kwetu ni mwendelezo wa hoja ya jana ya kupinga kauli ya Serikali juu ya matangazo ya TBC.
“Lakini hoja yangu ilikuwa kutaka kujua kama ni sahihi katika nchi kama Tanzania inayoheshimu haki za raia kuwanyima wananchi haki ya kupata habari.
“Lakini pia katika vurugu za jana, wapo wabunge wanawake waliporwa hereni na mikufu yao, lakini pia kuna waandishi wa habari walizuiliwa kutimiza majukumu yao, sasa yote haya ni sahihi?” alihoji.

NEWS:WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AKIONGOZA MBIO ZILIZOPEWA JINA LA "HAPA KAZI TU DODOMA HALF MARATHON" ZILIZOFANYIKA MJINI DODOMA LEO..


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongoza mbio za Wabunge za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon zilizoanzia Bungeni hadi uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Januari 30, 2016. Kushoyo kwake ni Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt Tulia Ackson. Mwansasu (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya Washiriki wa mbio za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon wakishiriki mbio hizo mjini Dodoma Januari 30, 2016.

Mmoja wa wapigapicha walioshiriki mbio za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon alilazimika kuomba msaada kwa askari wa usalama barabarani Mjini Dodoma Januari 30, 2016. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi ufunguo wa pikipiki mshindi wa kwanza wa mbio za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon upande wa wanaume, Emmanuel Giriki kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Januari 30, 2016.



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi zawadi ya Pikipiki mshindi wa kwanza upande wa wanawake wa Mbio za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon, Angela Davile (kulia) kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Januari 30, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Benki ya CRDB tawi la Dodoma ambao wamedhamini pambano la mpira wa miguu kati ya wabunge na benki hiyo kwenye uwanja wa Jamhuri Januari 30,2016. Benki hiyo pia ilitoa vifaa vya michezo kwa timu ya Bunge. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Powered by Blogger.
© Copyright JAMII YETU
Back To Top